Saturday, 16 December 2017

Vita Vizuri


Vita Vizuri


Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda. Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. 2 Timotheo 4:7,8


K
atika kipindi kirefu cha utumishi, kamwe Paulo hakusita katika utii wake kwa Mwokozi. Popote alipokuwa—iwe ni mbele za Mafarisayo wenye hasira, au mamlaka ya Kirumi; mbele za kundi lenye hasira pale Listra au wenye dhambi walioamini kwenye gereza la shimoni la Makedonia; iwe ni kutoa hoja kwa mabaharia walioshikwa na hofu kwenye mashua iliyovunjika, au kusimama peke yake mbele za Nero kutetea maisha yake—kamwe alikuwa hajawahi kujisikia kuaibika kutetea kile alichokiamini. Kusudi moja kuu la maisha yake ya Kikristo lilikuwa kumtumikia Yeye ambaye jina lake lilimjaza kwa dharau; na kutokana na kusudi hili, hakuna upinzani au mateso ambayo yaliweza kumgeuzia upande mwingine.

Maisha ya Paulo ni mfano wa ukweli aliokuwa akiufundisha na hapa ndipo tunapoona nguvu yake. Moyo wake ulikuwa umejawa na hisia yenye kina ya wajibu wake naye alifanya kazi kwa mawasiliano ya karibu zaidi na Mungu aliye chemchemi ya haki, rehema na kweli….Upendo wa Mwokozi ulikuwa ndiyo dhamira isiyokufa ambayo ilimshikilia kwenye mapambano yake dhidi ya nafsi na kwenye vita vyake dhidi ya uovu kama alivyokuwa kwenye utumishi wa Kristo akisonga mbele dhidi ya kutokuwa rafiki wa dunia na upinzani wa maadui zake.

Kile kanisa linachohitaji katika siku hizi za hatari ni jeshi la watendakazi ambao, kama Paulo, wamejifunza ili wawe wenye manufaa, ambao wana uzoefu wa kina katika mambo ya Mungu na ambao wamejawa na bidii na ari. Watu waliotakaswa, wanaojitoa wanahitajika; watu ambao hawatajitenga na majaribio na wajibu; watu walio jasiri na wakweli; watu ambao mioyoni mwao Kristo ameumbika “tumaini la utukufu,” naye ambaye midomo yake imeguswa kwa moto mtakatifu ata“lihubiri neno.”…

Je, vijana wetu watakubali hii amana takatifu itokayo mikononi mwa baba zetu? Wanajiandaa kujaza nafasi inayoachwa kutokana na kifo cha aliye mwaminifu? Maagizo ya mtume yatatiliwa maanani, mwito kwa ajili ya wajibu utasikiwa, katikati ya uchochezi wa ubinafsi na tamaa zinazowavutia vijana?

NENO LA MUNGU / 1 month ago

NGUVU YA ULIMI (MANENO) KATIKA KUAMUA HATMA YA MAISHA YAKO


Mada: Mambo muhimu kujua kuhusu matumizi ya kinywa
Katika sehemu ya kwanza nilikuonyesha mistari mbalimbali kutoka kwenye Biblia inavyozungumza kwa habari ya ulimi ili upate kujua nguvu ya ulimi ilivyo na athari zake. Ili kusoma sehemu ya kwanza tafadhali bonyeza link ifuatayo https://sanga.wordpress.com/2017/01/31/nguvu-ya-maneno-katika-kuamua-hatma-ya-maisha-yako-sehemu-ya-kwanza/
Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho nitafundisha mambo muhimu kuzingatia na kujua kwa habari ya matumizi ya ulimi (kinywa) ili kuweka hatma nzuri ya maisha yako kwa sababu maneno yako yana nguvu ya kuathiri maisha yako ya sasa na baadaye pia.
  • Jifunze kuzuia ulimi wako usinene mabaya – Mtume Petro anatueleza kwamba Kwa maana, Atakaye kupenda maisha, Na kuona siku njema, Auzuie ulimi wake usinene mabaya, Na midomo yake isiseme hila’ (1Petro 3:10). Ikiwa unataka kuwa na maisha yenye furaha na amani (siku njema) basi chunga sana unayoyasema. Ukiruhusu kinywa chako kunena mabaya na kutunga hila usitegemee kuwa na amani ya kweli, maana utaishi kwa maneno hayo. Daima usiakiache kinywa chako kinene mabaya wala kutunga hila kwa kuwa mtu azuiaye kinywa chake kunena mabaya, huilinda nafsi yake na taabu (Rejea Mithali 21:23 & Zaburi 50:19). Kumbuka unaponena mabaya juu ya mwingine, kama mtu huyo hana Yesu aliye hai wa kumuongoza kusamehe, basi ujue ndani yake unaamsha roho ya kisasi na uharibifu. Wapo pepo ambao kazi yao ni kufuatilia nini mtu anajinenea au kunena juu ya mwingine hususani yale ambayo ni mabaya, na kazi yao kufuatilia maneno hayo kuhakikisha kwamba yanatimia au yanatokea.
  • Jizuie kunena unapokuwa na hasira – Katika Waefeso 4: 26 imeandikwa Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka’. Mara nyingi kwenye jambo hili watu wengi wameshindwa kujizuia, na ukitaka ujue yaujazayo moyo wa mtu au mtu anakuwazia nini subiri azungumze habari zako au mambo yako akiwa amekasirika.  Hasira ni mlango ambao adui anautumia sana kuharibu maisha ya watu wengi na hasa wanandoa kwa sababu ya yale ambayo kila mmoja aliyanena akiwa na hasira na uchungu juu ya mwenzake. Biblia inatuambia kunyamaza ni hekima, hivyo jifunze kunyamaza. Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu’ (Mithali 17:28).

  • Jifunze kulinda kinywa chako – ukienda kwenye Mithali 13:3 Biblia inasema ‘Yeye alindaye kinywa chake hulinda nafsi yake, bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu’. Naam watu wengi hawajui kwamba kadri unavyosema maneno mabaya, ya uongo, kusengenya au kusingiza au kuchafua nk, ndivyo wanavyojitengenezea mazingira ya uharibifu kwenye maisha yao binafsi na si tu kwa wale ambao wanawaelekezea maneno husika.Katika Mithali 21:23 imeandikwa ‘Mtu azuiaye kinywa chake na ulimi wake, Atajilinda nafsi yake na taabu’Hii ni kwa sababu maneno unayoyanena unayaumba au kuyaandika na kwa jinsi hiyo maneno hayo yana nguvu ya kuongoza na kuathiri hisia, nia na maamuzi (matendo) yako.
  • Jifunze kuwa mtu wa maneno machache – Biblia inatuambia ‘Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili’ (Mithali 10:19). Naam sio lazima kusema kila neno linalokujia jifunze kunyamaza na kuzuia maneno yako, maana azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa. Ingawa Yakobo anatuambia ulimi haufugiki, lakini kwa mujibu wa (Mithali 17:27a) mtu anaweza kuzuia maneno yake na hiki ndicho alichomaanisha Mzee Yakobo mwenyewe pale aliposema iweni wepesi wa kusikia na si wepesi wa kusema (Yakobo 1:19).
  • Jifunze kufikiri kabla hujanena – Katika Mithali 12:18 imeandikwa ‘Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; Bali ulimi wa mwenye haki ni afya. Naamini umeshawahi kupitia mazingira ambayo unajutia maneno uliyoyanena. Mara nyingi majuto hayo ni matokeo ya kunena bila kufikiri. Hii ina maana kabla ya kusema, jifunze kufikiri kwanza athari ya unachotaka kusema kwa mtu au watu unaotaka kusema nao. Katika kufanikisha hili mwimbaji wa Zaburi akasema Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu’ (Zaburi 141:3).
  • Jaza neno la Mungu moyoni mwako (Yoshua 1:8) – Hii ni kwa sababu yale yaujazayo moyo wa mtu ndiyo yamtokayo. Hivyo ili kusaidia kinywa chako kutoa maneno yenye kujenga sharti neno la Mungu likae kwa wingi moyoni. Hatutegemei mtu aliyejaa neno la Mungu atukane watu, kulaani, kusengenya nk. Katika Yakobo 3:9-10 imeandikwa ‘Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo’. Naam ile kusema haifai mambo hayo kuwa hivyo ni ishara kwamba hatupaswi kutumia vinywa vyetu kunena mabaya na kutunga hila wakati tunatumia pia ulimi huo huo kumtukuza Mungu.
Katika kumalizia ujumbe huu sina budi kusema mwanadamu hana budi kuwa makini sana na kinywa chake. Maisha ya mtu yanachangiwa kwa sehemu kubwa na maneno yake, akiutumia vizuri ulimi wake  ataishi vizuri na akiutumia vibaya mabaya yatakuwa haki yake. Naamini ujumbe huu mfupi umekuongezea ufahamu wa kutosha mosi kuhusu Biblia inasema nini juu ya ulimi na pili namna ya kukitumia kinywa chako vizuri ili kuamua hatma nzuri ya maisha yako.
‘Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa’ (Zaburi 35:28)
Utukufu na Heshima vina wewe Yesu wangu, wastahili BWANA.
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, iwe nanyi.

“Hata sasa Bwana ametusaidia”


Mshukuruni Bwana,liitieni jina ,Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote. Zaburi 105:1, 2.

M
atendo ya Mungu kwa watu wake yapasa yatazamwe tena mara kwa mara. Ni mara ngapi Bwana aliweka alama njiani katika kushughulika na Israeli wa kale! Ili wasisahau historia ya wakati uliopita, alimwamuru Musa kuweka matukio haya katika mfumo wa wimbo, ili wazazi wapate kuwafundisha watoto wao. Iliwapasa wakusanye kumbukumbu na kuziweka kwa namna zinavyoweza kuonekana. Jitihada ya ziada ilifanyika ili kuyatunza, ili wakati watoto watakapouliza kuhusu mambo haya, kisa kizima kipate kuelezwa. Kwa namna hiyo, matukio yaliyotokea kwa wakati sahihi na wema bayana na rehema za Mungu katika uangalizi wake na ukombozi wa watu wake vilikuwa katika akili zao. Tunashauriwa hivi; zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu” (Waebrania 10:32). Bwana ametenda kama Mungu atendaye maajabu kwa ajili ya watu wake kwenye kizazi hiki… Mara kwa mara tunahitajika kukumbuka wema wa Mungu na kumsifu kwa sababu ya matendo yake ya ajabu.

Hebu tusitupilie mbali ujasiri wetu, bali tuwe na uhakika ulio imara, imara kuliko wakati wowote uliopita. “Hata sasa Bwana ametusaidia,” naye atatusaidia hadi mwisho (1 Samweli 7:12). Hebu tutazame vinara vya kumbukumbu, vinavyotukumbusha kile ambacho Bwana ametenda ili kutufariji na kutuokoa kutoka katika mkono wa mharabu. Hebu na tuweke upya katika kumbukumbu zetu rehema zote ambazo Mungu ametuonesha – machozi ambayo ameyafuta, maumivu ambayo ameyapoza, wasiwasi ambao amuondoa, hofu ambazo amezifutilia mbali, mahitaji ambayo ametupatia, baraka ambazo ametupatia - kwa namna hiyo tunajiimarisha wenyewe kwa ajili ya yote yaliyo mbele yetu kwa njia ya kumbukumbu za safari yetu.

Hatuwezi kuacha kutazama mbele kwenye fadhaa mpya za pambano linalokuja, lakini tunaweza kutazama kile kilichopita pamoja na kile kinachokuja, na kusema, “Hata sasa Bwana ametusaidia.” “Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako” (Kumbukumbu 33:25). Jaribu halitazidi uwezo tutakaokuwa tumepewa kulistahimili. Kwa hiyo, hebu tuchukue kazi yetu kuanzia pale tunapoikuta, tukiamini kwamba chochote kiwezacho kutokea, uwezo kulingana na jaribu utatolewa.